STAA wa Shindano la Big Brother, Mwisho Mwampamba, amesikitishwa na vitendo vya ubaguzi alivyofanyiwa na Polisi wa nchini Namibia, anakoishi na mkewe, Meryl Shikwambane, ambapo walimfuata kwenye nyumba yake na kumtaka aondoke nchini humo.
Mwisho ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, akisema nchi hiyo sasa hivi imekuwa kama Afrika Kusini, ambako wageni, hasa wenye ngozi ya Kiafrika, hupata shida ya kuishi kutokana na kubaguliwa.
“Mimi nimeoa mtu wao na nimezaa naye mtoto, nashangaa kubaguliwa na polisi hao, pia inashangaza kuona wakiwahudumia vyema wageni kutoka barani Ulaya, lakini sisi Waafrika wenzao tunabaguliwa,” alisema Mwampamba.
Mkali huyo ameshangazwa kupewa hati ya kuishi nchini humo kwa miezi miwili pekee, wakati ameoa mwanamke wa nchi hiyo, huku akipata shida hiyo hata mipakani.