Monday, September 23, 2013

LEWTHWAITE 'MJANE MWEUPE' ADAIWA KUHUSIKA SHAMBULIO LA KIGAIDI NAIROBI

 
Samantha Lewthwaite Mjane Mweupe' anayedaiwa kuhusika katika shambulio la Nairobi.
-Aliwahi kuja Tanzania akiwa na wanaye watatu
-Alikuwa mke wa Lindsay, mtuhumiwa wa ugaidi jijini London
-Alikuwa anatafutwa na polisi wa Kenya kabla ya tukio la juzi
-Al-Shabaab wamtaja kuwa mwanamke shujaa
-Alipanga kumtorosha mwenzake aitwaye Grant leo
Baadhi ya majeruhi katika shambulio la kigaidi jijini Nairobi.
Habari: Clarence Mulisa na Mitandao
MWANAMAMA Samantha Lewthwaite amehusiswa katika shambulio la kigaidi lililotokea jijini Nairobi,  juzi Jumamosi kwenye jengo la biashara la Westgate.
Lewthwaite amehusiswa kuwa miongoni mwa magaidi 10-15 wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo lililopoteza maisha ya watu 69 mpaka sasa wakati zaidi ya 175 wakijeruhiwa.
 
Mume wa Lewthwaite, Germaine Maurice Lindsay aliyeuawa watu 26 katika mlipuko wa Julai 7, 2015 jijini London.
Samantha Lewthwaite (29), maarufu kama 'Mjane Mweupe' ni Mwingereza aliyekuwa mke wa Germaine Maurice Lindsay maarufu kwa jina la Abdullah  Shaheed Jamal, mmoja wa magaidi kati ya wanne waliojitoa mhanga katika shambulio la Julai 7, 2005 jijini London lijulikanalo kama (7/7) lililouwa watu  56 pamoja na wao na kujeruhi zaidi ya 700.

Bomu la  Lindsay liliua watu 26 baada ya kulipua treni ipitayo chini ya ardhi jijini London.
Lewthwaite, ambaye alibadili dini enzi za ujana wake na kuitwa  Sherafiyah anadaiwa kuwa na watoto watatu.
Serikali ya Kenya imeeleza kuwa baadhi ya majeruhi waliookolewa kutoka katika jengo la Westgate walidai kumuona mwanamke mweupe (aliyefanana na Lewthwaite)  akiwa miongoni mwa magaidi walioteka jengo hilo.
Mabaki ya treni iliyolipuliwa na Germaine Lindsay na kuuawa watu 26.
Al- Shabaab kupitia katika akaunti yao ya Twitter wamemtukuza Lewthwaite kwa kusema yupo katika viwango vyao na ni  mwanamke shujaa.

Inasadikiwa kuwa mwanamke huyo alikuwa mmoja kati ya viongozi wa magaidi hao baada ya askari kudai kuwa mwanamke mweupe aliyekuwa amevaa hijabu alikuwa akitoa amri kwa wenzake katika lugha ya Kiarabu wakati wa shambulio hilo.

Desemba 2011, askari nchini Kenya walibaini kemikali za kutengeneza milipuko sawa na zile zilizotumika katika milipuko ya Julai 7, 2005 jijini London katika vyumba viwili vya kupangisha. Lewthwaite alidaiwa kuwa ndiye aliyekuwa amepangisha vyumba hivyo japo hakukamatwa.
Katika tukio hilo, Mwingereza, Jermaine Grant, alikamatwa akiwa jijini Mombasa kwa kuhusika na kemikali hizo. Baada ya kukamatwa, Grant aliwaeleza askari wa Kenya kuwa anafanya kazi chini ya Lewthwaite. Alikamatwa pamoja na mtu mwingine aliyekuwa anajaribu kutoroka nchini Kenya.
 
Habari iliyotolewa na gazeti la The Sun la Septemba 23, 2005 ikiwa na picha ya Lewthwaite akiwa amembeba mwanaye wa kike Ruqayyah, aliyezaa na Linsday.
Februari 2012, iliripotiwa kuwa mwanamke aliyekuwa akitumia vitambulisho mbalimbali kikiwemo cha Lewthwaite alikuwa anatafutwa na polisi wa nchini  Kenya, baada ya kugundulika hati feki ya kusafiria ya Afrika Kusini iliyokuwa na picha yake katika nyumba iliyohusishwa na vitendo vya kigaidi.
Aprili 2012, ilithibitishwa kuwa mtuhumiwa katika tukio hilo alikuwa Lewthwaite mwenyewe ambaye anadaiwa kuvuka mpaka wa Kenya na kuja Tanzania akiwa na watoto wake watatu Desemba 26, 2011.
                                Watoto wakiwa eneo lililoshambuliwa na magaidi.
Machi mwaka huu, Daily Telegraph liliripoti kuwa Lewthwaite na Fouad Manswab walikuwa wanapanga kumtorosha Grant na mpango wao ulipangwa kufanyika leo Septemba 23, 2013 jijini Mombasa.
"Tunajua Fouad anawasiliana na Samantha Lewthwaite na walipanga kumuokoa mwenzao," alisema Jacob Ondari,  Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa Kenya  kipindi hicho.
Katika ripoti mbalimbali, Lewthwaite anatajwa kuwa mfadhili, muongozaji na mwalimu wa al Qaeda na muandaaji wa Kundi la Jihad kwa wanawake barani Afrika.





Love to hear what you think!