Saturday, July 20, 2013

WASTARA: WALIONISAIDIA WANANITAKA KIMAPENZI

Stori:Gladness Mallya
Sura ya mauzo kunako gemu la filamu za Kibongo, Wastara Juma amefunguka kuwa wanaume wengi waliokuwa wakimsaidia wakati mumewe Juma Kilowoko ‘Sajuki’ akiwa mgonjwa wanamgeuka na sasa wanamtaka kimapenzi.
Akizungumza kupitia Kipindi cha Take-One katika Runinga ya Clouds chini ya Zamaradi Mketema, Wastara alisema baadhi ya watu ambao walikuwa karibu naye wakati Sajuki anaumwa sasa hivi wamegeuka na kumtaka kimapenzi, jambo ambalo linamuumiza na kumshangaza mno.
Bishosti huyo alisema kuwa tofauti na wanaume hao ambao walikuwa wakimpa sapoti kipindi hicho, bado wapo wengine kibao kutoka nje na ndani ya nchi ambao wanatuma maombi kwake lakini anawaona wote ni matapeli na wanamtamani tu hivyo hayupo tayari kuingia kwenye uhusiano wa aina hiyo.
“Kweli ninaumia sana kwa sababu ninakaa na kujiuliza hawa wanaume walikuwa wanasubiri mume wangu afariki dunia ndiyo wanitongoze?
“Kusema kweli inanishangaza, hata watu ambao sikuwadhania kabisa eti nao wananitaka, watu wajue kwa sasa sipo tayari kuwa na mwanaume.
“Sitaki kukurupuka kwa sababu naweza nikaingia kwenye shimo la taka kwani jamii itanikimbia kutokana na kunuka, natamani kumpata mwanaume anayefanana na mume wangu kitabia.
“Uvumilivu wangu na uzuri ulitokana na kutunzwa siyo aje mtu anayetaka nikavumilie shida, hilo sitaki litokee, namuomba Mungu sana,” alisema Wastara.
Kwa upande mwingine, staa huyo alisema kwa sasa yupo kwenye wakati mgumu kutokana na upweke na kama angekuwa hana watoto, angeomba afe akapumzike kwani faraja yake kubwa ilikuwa ni Sajuki lakini baada ya kutwaliwa na Mungu watoto ndiyo wamechukua nafasi hiyo.
Wastara aliwaomba watu wote wakimuona wasioneshe huzuni kwani ndiyo anaumia zaidi badala yake wawe na furaha kwani tangu aliporudi kutoka Uarabuni mawazo ya marehemu Sajuki yamekuwa yakimrudia mara kwa mara kutokana na kukutana na stori na maswali yaleyale.
Baadaye, Risasi Jumamosi liliwasiliana na Wastara na kumuuliza kama miongoni mwa wanaomtaka kimapenzi wapo wafanyakazi wa Global Publishers kwani ni miongoni mwa waliomsaidia ambapo alijibu kuwa hawahusiki.
“Jamani Global hamhusiki nilimaanisha mtu mmojammoja na wenyewe pia siyo wote ni baadhi yao,” alisema.
Wastara alifiwa na mumewe Sajuki Januari 2, mwaka huu baada ya kumuuguza kwa muda mrefu.




Love to hear what you think!