ASKARI Polisi wa Kituo cha Tarime mkoani Mara mwenye namba D. 4662
Koplo Mathew, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za uzembe uliosababisha
kifo kwa risasi cha mwanafunzi wa darasa la kwanza wa shule ya Msingi
Rebu, Deus Jacob (9).
Kifo hicho kilitokea wakati polisi wakiwa kwenye harakati za kukamata
mtuhumiwa, Marwa Bisara, mkazi wa kitongoji cha Songambele kata ya
Sabasaba mjini hapa, aliyekuwa akituhumiwa kwa shambulio na kudhuru
mwili.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, alisema
jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 10 jioni katika kitongoji cha
Songambele, baada ya Koplo Mathew na askari wenzake wakiwa na
mlalamikaji, wakifuatilia mtuhumiwa na kumkuta na wenzake katika pagala
wakivuta bangi.
Wakati polisi wakijiandaa kumkamata, mtuhumiwa Bisara alimvamia Koplo
Mathew akitaka kumnyang'anya bunduki na katika purukushani hiyo, risasi
zilifyatuka na moja kumpata Deus kichwani na kumuua papo hapo baada ya
kichwa kufumuka.
Kamanda Kamugisha alisema chanzo cha mauaji ni mtuhumiwa Bisara
kukaidi amri ya kukamatwa. Lakini mwenzake Julius Maseke (38) mkazi wa
mtaa wa Ronsoti alikamatwa akiwa na misokoto 47 na kilo 3.25 za bangi na
anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Polisi ilitoa mwito kwa raia wema kutoa taarifa kwa vyombo husika watakapomwona Bisara na inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele alionya wanasiasa waache
kulitumia tukio hilo kisiasa kwa kuwa marehemu Deus hakuwa mwanachama wa
chama chochote cha siasa.
Alionya hivyo kwa alichokisema ni baadhi ya
wafuasi wa Chadema kuchocheana kufanya vurugu wakihamasishana kuchukua
mwili wa marehemu huyo na kufanya maandamano kwenda Bomani ziliko ofisi
za Mkuu wa Wilaya na Kituo cha Polisi.
Hata hivyo, maandamano hayo
yalizimwa na Polisi kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi na mwili huo uko
katika mochari ya hospitali ya wilaya na unatarajiwa kuzikwa leo.