Walisema kuwa ingawa bado hakuna visababishi
kamili vya saratani hiyo, asilimia 90 ya wagonjwa wa saratani ya koo
wamekuwa na historia ya uvutaji sigara, unywaji pombe kali kama viroba
na kula aina za vyakula vilivyochomwa ikiwamo nyama na samaki, ulaji
pilipili, ndimu, ‘chilisosi’ na unywaji wa vitu vya moto kupita kiasi.
“Ongezeko ni kubwa, asilimia 90 ya wagonjwa
tuliowapokea hapa wana historia ya kutumia vilevi vikali, sigara,
pilipili kwa wingi na aina nyingine na vitu vinavyosababisha saratani
hii,” anasema Dk Kahesa.
Anasema kuwa Saratani ya Koo ni mbaya zaidi ukilinganisha na saratani za aina nyingine.
Anaeleza: “Saratani ya Koo ni mbaya ukimwona
mgonjwa unaweza kulia, hawezi tena kula na ikibidi huingiziwa mipira
maalumu ili kupitisha chakula, lakini kuna wakati hata mipira huziba,
hivyo huishi kwa dripu ya chakula pekee.”
Naye Dk Mwakyoma anaeleza kuwa Saratani ya Koo
hushambulia seli zinazotanda koo na kutengeneza uvimbe katikati ya koo
ambao huanza kuleta madhara taratibu.
“Ukiwa na Saratani ya Koo, itakuchukua muda mrefu
sana mpaka kuanza kuona viashiria mbalimbali, awali mgonjwa huanza
kupata shida kumeza chakula. Wengi hufika hapa wakiwa wamechelewa na
tunavyofanya vipimo huwa katika hatua mbaya sana,” anasema Mwakyoma.
Anazitaja aina kuu mbili za Saratani ya Koo kuwa
ni: “Oesophagus Carcinoma na Squamous cell carcinoma, ambazo
hutofautiana kulingana na jinsi seli zake zinavyoonekana kwenye
darubini.
Hata hivyo, pamoja na tofauti hizo za mwonekano, utambuzi na matibabu ya aina hizi za Saratani ya Koo hufanana.”
Anabainisha kuwa aina zote mbili huanza kwa
kuathiri seli zilizo katika utando wa ndani wa ukuta wa koo, uitwao
‘mucosa’ kabla ya kusambaa maeneo mengine.
Kwa upande wake Dk Kahesa anasema kuwa katika
hatua za awali, mgonjwa mwenye Saratani ya Koo anaweza asionyeshe dalili
zozote. Hata hivyo, kadiri saratani inavyozidi kukua na kuenea, mgonjwa
anaweza kuanza kuona dalili.
“Dalili ya kwanza ya mgonjwa wa saratani ni
chakula kukwama kwenye koo, siku za mwanzo mgonjwa anaweza kushindwa
kumeza chakula kigumu kisha cha majimaji na baadaye akashindwa kumeza
hata mate.