SHEREHE za miaka 36 za kuzaliwa kwa CCM jana ziliingia dosari,
baada ya kuibuka vurugu kubwa kati ya wafuasi wa chama hicho na Chadema
mkoani Dodoma wakati wakigombea eneo na mti wa kutundika bendera za
vyama vyao.
Vurugu hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza
Ghasia (FFU), zilitokea jana mchana katika uwanja huo uliopo karibu na
Baa ya Mwanga, baada ya CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwepo
uwanjani hapo, ili waweke bendera zao kwa ajili ya mkutano ambao ulikuwa
sehemu ya maadhimisho hayo.
Vurugu zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema
kuwataka wenzao wa CCM waendelee na mkutano katika eneo hilo kwa sharti
la kurejeshwa kwa bendera iliyong’olewa. Wafuasi wa vyama hivyo wakiwamo
wabunge wa CCM walionekana wakivutana kunyang’anyana mti wa bendera.
“Baada ya CCM kugoma, Chadema walijaribu kurudisha
bendera hiyo kwa nguvu, jambo ambalo lilifanya wafuasi wa CCM waanze
kuokota mawe na kuwarushia wapinzani wao hao, huku Chadema nao walianza
kujibu mapigo,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Baadhi ya wabunge wa CCM walioshiriki katika
vurugu hizo na majimbo yao kwenye mabano ni Ismail Aden Rage (Tabora
Mjini), Nyambari Nyangwine (Tarime), Seleman Jafo (Kisarawe), Said
Mtanda (Mchinga) na Mary Chatanda (Viti Maalumu).