Scina Mlewa akiwa na majeraha baada ya kumwagiwa uji wa moto na mke wake aitwae Habiba Shomari.
SCINA Mlewa (28) amejikuta akilia baada ya mke wake aliyetajwa kwa jina la Habiba Shomari kudaiwa kumwagia uji wa moto uliokuwa ukichemka jikoni.
Akisimulia tukio hilo huku akilia, Mlewa alikuwa na haya ya kusema:
“Mimi ni dereva wa daladala linalofanya safari Mwenge na Temeka, Septemba 28, mwaka huu sikuweza kurudi nyumbani baada ya basi hilo kuharibika. Kutokana na tatizo hilo, nilishindwa kuliacha barabarani ndipo nilimtumia ujumbe mke wangu kumuarifu.
Scina Mlewa akiwa na huzuni baada ya kuunguzwa kwa uji wa moto na mkewe.
“Niliporudi nyumbani asubuhi nilikumbana na maswali mengi kutoka kwa mke wangu, kisha akaingia jikoni na kunyanyua surufia iliyokuwa na uji akanimwagia usoni, ukaniunguza vibaya sana.
“Baada kufanyiwa unyama huo nilipiga mayowe ya kuomba msaada ndipo wasamaria walikuja na kunipeleka Hospitali ya Temeke ambako nililazwa.
“Kabla ya tukio hilo tumekuwa tukizozana mara kwa mara na hata kutishia maisha yangu lakini nashindwa kuachana naye kwa kuwa nimezaanaye,” alilalamika Mlewa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, ACP David Misiime amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mama huyo ameshakamatwa na upelelezi unaendelea.