Wednesday, July 11, 2012

Sumatra yapika nauli mpya za daladala


0digg
Aidan Mhando
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesema ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kupitia maoni ya wadau wa usafiri kuhusu mapendekezo ya kuongezeka kwa nauli mpya za daladala.

Hayo yalibainishwa jana na Ofisa Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kuhusu hatua ambazo Sumatra imefikia baada ya wamiliki wa daladala (Dacoboa), kupendekeza kuanza kutumika kwa nauli mpya za daladala kutoka Sh350 hadi 870.

Alisema kazi ya kupitia maoni na mapendekezo ya wadau wa usafiri kuhusu kuanza kutumika kwa nauli mpya za daladala unaendelea na kwamba upo katika hatua za mwisho kukamilika.

“Kwa sasa Sumatra haiwezi kusema chochote kuhusu lini nauli mpya za daladala zitaanza kutumika kwani  mchakato wa kupitia maoni na mapendekezo ya wadau unaendelea lakini ninachoweza kusema umefikia katika hatua nzuri,” alisema Mziray.

Alifafanua kuwa wakati mchakato huo utakapo kamilika bodi ya Sumatra itakutana na kuamua nini kifanyike kwa kupitia mambo yote yaliopendekezwa kwani wao ndio watakuwa waamuzi wa mwisho katika suala hili kama nauli mpya za daladala zitaanza kutumika au nauli za awali zitaendelea kutumika.

Mei 24 mwaka huu wadau wa usafili walikutana jijini Dar es Salaam na kujadili mapendekezo yaliowasilishwa na Dacoboa ya kutaka  kuongezeka kwa nauli za daladala kutoka Sh 350 hadi 870.



Love to hear what you think!