*NI KATIKA MKUTANO WA MNYIKA,MWENYEKITI WA KATA UVCCM AUAWA,18 WAJERUHIWA
Raymond Kaminyoge, Dar na Gasper Andrew, Singida VURUGU kubwa zilizotokea kwenye mkutano wa hadhara zikiwahusisha wafuasi wa Chadema na CCM zimesababisha kifo cha Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wa Kata ya Ndago, wilayani Iramba, Yohana Mpinga (30) na majeruhi mmoja.Wafuasi hao wa Chadema na CCM walishambuliana kwa kutumia silaha za jadi ikiwamo mawe, wakati wa mkutano wa hadhara uliokuwa unahutubiwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kifo cha mwenyekiti huyo baada ya kupigwa kwa silaha za jadi.Kamanda Sinzumwa alifafanua kwamba, kutokana na tukio hilo, jeshi hilo linawashikilia watu 18 wa kata hiyo kwa mahojiano zaidi na watakapobainika kuhusika na ghasia hizo watafikishwa mahakamani.Alisema majeruhi huyo wa vurugu hizo anayejulikana kwa jina la Ramadhani Hussein (27), amelazwa katika Kituo cha Afya cha Ndago baada ya kujeruhiwa vibaya.
“Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Julai 14 mwaka huu saa 10 alasiri katika Kijiji cha Ndago,” alisema Kamanda.Alisema siku ya tukio, Chadema kilikuwa na kibali cha kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji hicho na mgeni rasmi alikuwa Mbunge Mnyika.Kamanda Sinzumwa alisema kuwa, baada ya Chadema kuanza mkutano huo, viongozi wake walianza kutoa kashfa mbalimbali dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi (CCM), Mwingulu Nchemba.
Alisema kitendo hicho kiliwaudhi baadhi ya watu waliokuwa wamehudhuria mkutano huo."Wananchi hao walichukizwa na kitendo cha kukashifiwa mbunge wao na walianza kupiga kelele kuwa hawataki mbunge wao akashifiwe na badala yake, wakawataka Chadema wawe wanaeleza sera zao na si vinginevyo,” alisema.Kamanda huyo alisema licha ya tahadhari hiyo, viongozi hao waliendelea kueleza kashfa za Mbunge Nchemba na ndipo vurugu zilipoanza.
Alifafanua kwamba, vurugu hizo zilianza baada ya wafuasi wa CCM waliokasirishwa na kashfa zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa Chadema kuanza kuwarushia mawe wafuasi wa Chadema. Kamanda Sinzumwa alisema askari polisi wachache waliokuwapo, walizidiwa nguvu na makundi hayo."Huyu Mwenyekiti wa Vijana wa CCM, Yohana alikimbilia kwenye nyumba ya Mwalimu Shume Manase ili kuokoa maisha yake, lakini kundi la wafuasi wa Chadema wakiwa wamebeba fimbo na mawe, walimpiga sehemu mbalimbali mwilini na kusababisha kifo chake papo hapo," alisema.
Kamanda huyo alisema licha ya watuhumiwa 18 kukamatwa, polisi bado inaendelea na msako wa kuwatafuta watu wengine waliohusika katika tukio hilo ili wafikishwe mahakamani.Kauli ya MnyikaAkizungumzia vurugu hizo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema mbinu chafu zinazotumiwa na CCM za kupiga mawe mikutano yao ya hadhara kamwe haitakidhoofisha chama chao katika harakati zake za kuwakomboa wananchi kutoka katika maisha magumu.
Mnyika alisema amefurahi kufika katika jimbo hilo la Mbunge Nchemba kwa sababu ya propaganda zake, ambazo amekuwa akizitoa bungeni na alivyofanya ziara kwenye jimbo lake la Ubungo na kuwahutubia watu wa Manzese.Mnyika alisema wakati wowote kuanzia sasa viongozi wa juu wa chama hicho watafanya ziara kwenye kata zote za Mkoa wa Singida ili, kuwafahamisha wananchi hatua za kuchukua katika uchaguzi ujazo.
Nape akataa kuzungumziaAkizungumzia suala hilo kwa simu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema suala la mauaji lisifanywe kuwa la kisiasa.“Mnataka niseme nini wakati wauaji wanafahamika? Mtafuteni Kamanda wa polisi awaeleze kuhusu tukio hilo na hatua zilizochukuliwa, suala hili tusilifanye kuwa la kisiasa,” alisema Nnauye alipotakiwa kutoa maoni yake.
Mnyika na Nchemba Mvutano wa wabunge hao lilianza hivi karibuni bungeni baada ya Mnyika kumtuhumu Nchemba kwamba, ni mmoja wa watuhumiwa wa wizi wa Sh133 bilioni za Akaunti za Madeni ya Nje (EPA) uliotokea katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).Kombora hilo la dhidi ya Nchemba ambaye pia ni Mweka Hazina wa CCM, lilisababisha mabishano bungeni yaliyodumu kwa dakika 20.
Mnyika alirusha kombora hilo baada ya Nchemba kuchambua bajeti kivuli ya upinzani kuhusu Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora) na kukosoa baadhi ya maneno ikiwamo hoja ya kuwa, walimu wanafanya biashara shuleni kitu akisema kuwa huo ni udhalilishaji wa wanataaluma hao.
Kombora hilo la Mnyika lilimsimamisha Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama ambaye alimpa Mnyika siku saba kutoa uthibitisho wa tuhuma alizozitoa dhidi ya Nchemba.Mnyika alifanya hivyo lakini, Naibu Spika Job Ndugai alisema kuwa, ushahidi uliotolewa na mbunge huyo hauna mashiko hivyo kulipeleka suala hilo mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka.E&P