CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema
hakiwezi kukubali viongozi wake wanaodaiwa kutishiwa maisha kuhojiwa na Jeshi
la Polisi kama imevyoelekezwa na Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi kwani hawana imani na Polisi. Kauli hiyo imetolewa leo na
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Peter Slaa alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Peter Slaa alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Akitoa tamko hilo ambalo limepitishwa
na Kikao cha Kamati Kuu iliyokutana tangu juzi, Dk. Slaa amesema hawaoni sababu
ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa kuwa wamewahi kuwapa taarifa nyingi za
vitisho dhidi yao
na hakuna hata moja imefanyiwa kazi.
“Hatuwezi kwenda Polisi kwa sababu tumekuwa tukipeleka mambo
mengi ya vitisho lakini hayafanyiwi kazi…na hili tulisha waambia hatuendi kwao
labda watukamate,” alisema Dk. Slaa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema yeye mwenyewe licha ya kuwasilisha madai mbalimbali
aliwahi kutegeshewa vinasa sauti na kutoa taarifa polisi lakini tangu wachukue
vifaa hivyo hawajasema chochote hadi leo, jambo ambalo limewafanya waamini hata
wakienda huko hakuna chochote kitafanyika.
Dk. Slaa alisema leo asubuhi alipigiwa simu na mmoja wa
maofisa upelelezi kutoka Makao Makuu ya Polisi akiomba miadi ya kukutana naye,
jambo ambalo amesema hayupo tayari kuhojiwa na wanausalama hao wa raia labda
wamkamate.
Alisema tayari baadhi ya viongozi wa Serikali wameanza
kuipuuza malalamiko yao dhidi ya vitisho wakidai huenda viongozi wa CHADEMA
wanatafuta umaarufu wa kisiasa kwa kutoa taarifa hizo, kitendo ambacho amesema
umaarufu wao hautatokana na viongozi wa Serikali au CCM bali ni kwa kazi
wanazozifanya kwa wananchi.
Juzi Dk. Nchimbi alisema taarifa za kutishiwa maisha dhidi
ya viongozi wa CHADEMA ni nzito hivyo haziwezi kupokelewa kirahisi Jeshi la
Polisi linaanza kazi ya kuwahoji wahusika ili kulifanyia kazi jambo hilo. Alisema suala la
usalama wa raia si hiyari bali ni la lazima hivyo hata kama
wahusika hawataki lazima taratibu zifanywe kuhakikisha usalama kwa wahusika.
Wakati huo huo CHADEMA inaanza ziara ya Oparesheni Sangara
ambayo itafanyika katika mikoa mitano ya Tanzania
ikiwemo Dodoma,
Morogoro, Iringa na Manyara. Akizungumzia ziara hiyo ambayo itashirikisha
viongozi wa juu wa CHADEMA, Wabunge, Wajumbe pamoja na viongozi wengine wa
ngazi mbalimbali. Dk. Slaa amesema ni ziara ya kukiimarisha chama ikiwa ni
pamoja na kuangalia mchakato wa uchaguzi wa chama hicho unaoendelea ngazi za
chini.
Alisema katika ziara hiyo ambayo kauli mbiu yake ni “Hakuna
Kunywa, Kula wala Kulala” inatarajiwa kuzunguka katika majimbo ya uchaguzi 44
ya mikoa hiyo, Kata 806 na vijiji 4,000. Ziara hiyo inatarajia kutumia siku
104.
Akifafanua zaidi kuhusiana na ziara hiyo amesema CHADEMA ni
chama ambacho kinajitofautisha na vyama vingine katika utendaji wake na ndiyo
maana wanaendelea kufanya ziara zao vijijini kuangalia maisha ya wananchi
mpango ambao ni mpya.
“Kuna taarifa za baadhi ya watu wanabeza ziara zetu kwamba
zinalenga posho…no CHADEMA hakuna posho, kwenye ziara zetu tunakula hadi kwa
mama ntilie (chakula cha kawaida), tutaendelea kupiga kelele hadi pale haki za
Watanzania zitakapokuwa zikipatikana bila vikwazo…tunapigania haki ya kila
mmoja awe mwanafunzi, wafanyakazi, wakulima na hata madaktari,” alisema Dk.
Slaa.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com
(www.thehabri.com)