Pamoja na watu kuwa wengi hadi wengine kurudishwa nyumbani, lile Tamasha la Wafalme limekamilika na shoo kabambe iliyotolewa na wafalme wawili, mkali wa Afro Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye kila mtu alikubali kwamba hakuna kama yeye Bongo na mfalme Mzee Yusuf.
Shoo hiyo ya kihistoria ilifanyika usiku wa kuamkia jana katika Mkesha wa Sikukuu ya Krismasi kwenye Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.
MWANZO WA SHOO
Shoo iliyoshuhudiwa na mapaparazi wetu, ilianzia kwa waimbaji wa Kundi la Jahazi Modern Taarab ambao walitoa burudani za mwanzo huku wakiimba nyimbo mbalimbali zikiwemo zile zilizopo kwenye albam yao mpya inayojulikana kwa jina la Chozi la Mama.
MZEE YUSUF
Jahazi waliimba nyimbo nyingi kabla ya mfalme mwenyewe Mzee Yusuf hajapanda stejini.
Alipanda stejini saa 6:04 usiku ambapo kelele zilitawala huku mashabiki wakimwita babu..babu... babu... na kuanza rasmi kwa kupiga gitaa la besi kwa takribani dakika 16 na baadaye alihamia kwenye kinanda huku mkewe Leyla Rashid ‘Malkia’ akiimba na kuoneshana mahaba niue.
Mashabiki walifurahi zaidi pale mfalme huyo alipopanda mwenyewe na kuanza kuimba nyimbo mbalimbali ikiwemo Daktari wa Mapenzi, Chozi la Mama, Wabaya Waulizane, Wasiwasi Wako na nyingine nyingi.
MFALME DIAMOND
Baada ya Mzee Yusuf ambaye alidhihirisha kuwa ni mkali na kuweka rekodi yake, shangwe kubwa liliibuka pale Diamond alipopanda stejini, ilikuwa saa 7:38 usiku na kuanza kufanya yake kama ilivyo kawaida mashabiki walimpokea kwa kumuita afande.
Diamond alianza kutoa shoo kwa kupiga baadhi ya nyimbo zake, Kam wambie, Nitarejea, Mdogomdogo, Ntampata Wapi na nyingine nyingi kama ‘play back’ na kuhamia kwenye ‘live band’ ambapo aliimba nyimbo za Mawazo, Moyo Wangu na Nimpende Nani na kufuatiwa na sebene la nguvu.
Diamond hakuishia hapo, alikuja na ‘sapraiz’ kwa mashabiki kwa kumpandisha jukwaani Mshindi wa Shindano la Big Brother Africa ‘Hotshots’ 2014, Idris Sultan ambaye alitoa shukrani kwa mashabiki:
“Kile nilichokuwa nikiahidi kwa mashabiki ambao walikuwa wakinipigia kura sasa ndiyo naanza kutekeleza kama ifuatavyo, na leo nimekuja hapa kwenu kutoa shukrani zangu za dhati.“Ninaomba nimtambulishe mshiriki mwenzangu kutoka Afrika Kusini, Samantha (shori mkali) ambaye ndiye rafiki yangu.
“Ametoka huko (Afrika Kusini) kuja kunipa sapoti hapa kwetu Tanzania, nawashukuru sana Watanzania wenzangu bila ninyi mimi si chochote lakini ushindi ni wa kwetu wa tuzo tatu za MTV (alizochukua Diamond) na dola laki tatu za BBA (alizolamba yeye) hatutaishia hapa, tutaendelea kusonga mbele,” alisema Idris na kuibua bonge la shangwe.
NAFASI YA NAY WA MITEGO
Baada ya tukio hilo, Diamond aliendelea kufunika kuimba kwa kumtaka mtu ambaye atachukua nafasi ya mwanamuziki mwenzake, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ kwenye Wimbo wa Muziki Gani ambapo alijitokeza kijana aliyejitambulisha kwa jina la Sadiki Juma aliyekamua vilivyo kipande hicho na mwisho Diamond alimkubali kuwa anaweza muziki na kumpa zawadi ya shilingi elfu hamsini na kumkabidhishwa kwa meneja wake, Babu Tale.
SEBENE
Diamond alipagawisha zaidi kwa kutoa shoo ya sebene kwa mashabiki wake huku akiwaita baadhi ya watu kwenda kutoa shoo ambapo walianza wacheza shoo wake, yeye mwenyewe, Babu Tale, Mkubwa Fela na wengine kibao.
ZARI AMFUNIKA WEMA
Katika hali ya kushangaza, muda wote mashabiki hao waliorundikana Dar Live hadi polisi wakazuia ukatishaji wa tiketi getini wakiwataka watu kurudi nyumbani, walikuwa wakipiga kelele wakimtaka Diamond amlete stejini msanii wa uganda, Zarinah Hassan ‘Zari’ anayedaiwa kutoka naye kimapenzi huku wachache wakimshabikia Wema Sepetu ‘Madam’, aliyekuwa mpenzi wa Diamond.Imeandaliwa na Shani Ramadhani, Mayasa Mariwata, Musa Mateja na Issa Mnally