Wednesday, September 25, 2013

Wanasheria waenda kuvunja mkataba wa Okwi

Kiungo mshambuliaji wa Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, Emmanuel Okwi.
Na Joan Lema
KIUNGO mshambuliaji wa Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, Emmanuel Okwi, yupo katika hatua za mwisho za kuvunja mkataba na timu hiyo.
Okwi ameamua kufanya hivyo baada ya kuona timu hiyo inakiuka vipengele vilivyo katika mkataba kati ya pande hizo mbili.
Raia huyo wa Uganda yupo hapa nchini tangu wiki iliyopita kwa ajili ya matembezi na amekuwa kwao Kampala kwa zaidi ya wiki tatu sasa baada ya kususia kurejea Sousse, Tunisia.
Akizungumza na Championi Jumatano, rafiki wa karibu wa kiungo huyo mshambuliaji ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini, alisema Okwi kwa sasa ameshazungumza na wanasheria wake ili aweze kuvunja mkataba na klabu hiyo.
“Ameamua kuvunja mkataba, hajalipwa mshahara wa miezi minne sasa. Kama hiyo haitoshi hata fedha yake ya kusaini mkataba hajamaliziwa. Tayari amezungumza na wanasheria na atavunja mkataba,” alisema.
Aliongeza kuwa, kwa sasa Okwi mawazo yake yapo katika kuuvunja mkataba huo ili abaki huru na hajajua ni timu gani ataichezea baada ya kufanikisha suala hilo.
Alipofuatwa na Championi Jumatano, Okwi alikiri kuanza mazungumzo hayo lakini akasisitiza hatakuwa tayari kulizungumzia hadi hapo baadaye.
“Nisingependa kulizungumzia hilo suala kwa sasa, tafadhali naomba unielewe,” alisema Okwi.
Simba ilimuuza Okwi kwa dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 480).





Love to hear what you think!