Na Siafel Paul
STAA wa filamu za Kibongo asiyekaukiwa vimbwanga, Wema Isaac Sepetu amezua bonge la timbwili kwa wafanyakazi wake wa ndani wa kiume na kike akiwemo mlinzi, Amani linakuletea kisa na mkasa.
Tukio hilo lililonaswa na vifaa vyetu vya kisasa vya kunasia matukio ya mnato na video, lilijiri juzikati nyumbani kwa mwanadada huyo, Kijitonyama, jijini Dar na kusababisha majirani kufaidi sinema ya bure ya matusi ya nguoni.
ILIKUWAJE?
Ilikuwa majira ya asubuhi ambapo Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006/07, akiwa ametinga dela, nywele bandia nyekundu na miwani nyeusi, alikuwa amejiandaa kwa ajili ya mtoko lakini alipoingia kwenye gari lake aina ya Toyota Lexus Harrier ndipo akagundua tatizo.
Cha kwanza alichogundua ni kwamba gari hilo lilikuwa limeibiwa power window (mashine ya kushusha na kupandisha kioo) zote.
Cha pili ni kwamba alipopiga ‘stati’ gari hilo lilikataa kuwaka kutokana na kuchokonolewa kwenye betri.
Baada ya kuona hivyo, Wema aliwaita wafanyakazi wake wawili, mmoja wa kiume na mlinzi na kuanza kuwawashia moto kuwa walikuwa wakijua kilichoendelea.
APANDWA NA HASIRA
Wema alianza kuwahoji kuwa walilifanya nini gari hilo, waliponyamaza kumjibu ndipo akapandwa na hasira na kuanza kutoa mkong’oto kwa kutumia chochote alichokutana nacho mbele yake.
MITUSI MIZITO
Huku akimmwagia maji machafu yule mlinzi wa kiume na kumpiga kwa dekio la plastiki, Wema alikuwa akimwaga mitusi mizito ya nguoni isiyoandikika gazeti kutokana na ukali wake.
“My friend ninyi ni mabogasi kabisa, nawaambia mtaozea Segerea, mnafanya nini hapa ninyi wa…(tusi) au mna…(tusi kali).
“Ninyi ni …(tusi kubwa likihusisha mama zao), mnakaakaa tu hapa wa…(tusi tena), mnajua bei ya power window? Mnadhani hili ni Toyota? Kwa taarifa yenu hili ni Lexus …(tusi) zenu,” alisikika Wema akitumia lugha ya matusi ambayo asilimia kubwa hayaandikiki kwa namna yoyote kutokana na kupitiliza.
Wema aliendelea kuwakimbiza ndani ya fensi akiwapiga huku sauti ya Martin Kadinda (yule meneja wake) ikisikika, ‘Mwache ataruka ukuta, nenda karipoti polisi’.
AMGEUKIA FIONA
Huku akiwa mbogo, Wema alimgeukia mmoja wa mbwa wake aitwaye Fiona na kumuwashia moto huku akimmwagia mitusi:
“Na wewe Fiona unakaa hapo hapo unamuuzia nani sura badala ya kulinda mlinzi, sipendi mambo ya ki… (tusi).
NI HUJUMA?
Mkurugenzi huyo wa kampuni ya kufyatua filamu ya Endless Fame Production alikwenda mbali na kuwatuhumu wafanyakazi hao kuwa kuna uwezekano wanatumiwa kumhujumu akiahidi kuwakomesha.
“Mnatumwa mnapewa pesa ili mnifanyie hivi…gari litaibiwaje power window likiwa ndani na ninyi mkiwepo? Wa…(tusi) sana ninyi,” alisikika msanii huyo.
Katika hali ya kushangaza, badala ya kumuwashia moto mlinzi anayehusika na usalama nyumbani hapo, Wema ‘alidili’ na wafanyakazi wa ndani tu huku mlinzi naye akishindwa kumuamulia na kubaki kumtazama tu namna alivyokuwa akikimbizana na wafanyakazi hao.
NENO LA MAJIRANI
Kwa upande wao majirani walikuwa wakila chabo na kusikitishwa na mvua ya matusi aliyokuwa akiitoa msanii huyo ambaye ni kioo cha jamii.
“Jamani jamani, hivi hajui tuna watoto wadogo ambao hawastahili kusikia matusi makubwa kama anayomwaga?
“Ukweli Wema anatusikitisha sana kwa sababu watoto wanajifunza nini kutoka kwake?” alihoji mmoja wa majirani hao aliyeomba hifadhi ya jina ili na yeye asije akawashiwa moto na msanii huyo.
AMANI LAFUNGASHA VIRAGO
Hadi Amani linafungasha virago maeneo hayo mwanadada huyo alikuwa akijiandaa kwenda kuripoti tukio hilo polisi hivyo tunaendelea kufuatilia kilichojiri.