MALKIA wa Muziki wa Taarab nchini anayelitumikia Kundi la Tanzania One Theatre (TOT), Khadija Omary Kopa inadaiwa kuwa alianza kuona maruweruwe na kukosa usingizi kabla ya kupewa taarifa za kifo cha mumewe ambaye ni Diwani wa Kata ya Magomeni Wilayani Bagamoyo, Jafary Ally.
Kopa aliyekuwa mkoani Rukwa na Kundi la TOT kwa ajili kutumbuiza kwenye ziara ya Makamu wa Rais, Dokta Mohammed Ghalib Bilal, alikumbwa na maruweruwe usiku kucha wakati mumewe akiteseka na kukata roho kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa rafiki wa Kopa aliyekuwa Rukwa, usiku wa kifo cha mumewe, malkia huyo alikosa usingizi na kukumbwa na maruweruwe mpaka walipopokea taarifa za kifo cha mwanaume huyo.
“Niko naye jirani, hana nguvu za kuweza kuzungumza lakini tupo Arusha tumeletwa na ndege ya makamu wa rais, tunasubiri ndege nyingine ya kutupeleka Dar es Salaam na kuelekea Bagamoyo kwa ajili ya mazishi,” alisema rafiki huyo wa Kopa.
Akizungumza na gazeti hili, mama mzazi wa marehemu ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kata ya Tandale jijini Dar, Rehema Tuwa amesema amepata pigo kubwa la kuondokewa na mwanaye tegemezi.
“Kinachoniuma zaidi ni mwanangu kufariki dunia ghafla, Jumatatu tulimkimbiza hospitali kutokana na homa kali, ghafla usiku wa kuamkia leo (juzi) nashangaa kupewa taarifa za kifo, inaniuma sana,” alisema.