Saturday, May 4, 2013

NDEGE ZA PRECISION AIR ZAPIGWA 'STOP' KURUKA AU KUTUA ZANZIBAR.

Moja ya ndege za Precision Air ikiwa angani katika moja ya safari zake.
Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB), imetoa amri ya kuzuia kutua na kuruka kwa ndege za kampuni ya Precision Air Service Co. Ltd, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, kutokana na kutolipa zaidi ya Sh bilioni 37.2 zinazotokana na malimbikizo ya malipo ya ada ya huduma ya uwanja wa ndege.
Amri hiyo iliyopatikana jana, imetolewa na Kamishna wa Bodi ya Mapato ya Zanzibar, Abdi Faki, Aprili 25 mwaka huu kutokana na malimbikizo hayo.
“Chini ya kifungu cha 43(1) cha taratibu na udhibiti wa kodi cha mwaka 2009, mimi Abdi Faki, Kamishna wa Bodi ya Mapato ninatoa amri ya kuzuia kuruka na kutua kwa ndege za kampuni ya Precision Air Service Co. Ltd kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kuanzia saa saba usiku wa Aprili 25 mpaka hapo watakapolipa fedha hizo.”
Mbali na amri hiyo, pia ZRB inakusudia kufunga ofisi zote za kampuni hiyo zilizopo Zanzibar.
Faki alisema kuwa Precision Air Service Co. Ltd, imeshindwa na kupuuzia kulipa deni la zaidi ya Sh milioni 144.8 na zaidi ya dola za Marekani 347,066 (zaidi ya Sh milioni 520.6), kama malipo ya makato ya huduma za viwanja na usalama kwa miezi mitatu tangu Januari hadi Machi mwaka huu.
Alisema pia kampuni hiyo imeshindwa kulipa zaidi ya Sh milioni 70.5 na zaidi ya dola za Marekani milioni 1.6 (zaidi ya Sh bilioni 2.5), kama fedha za adhabu kutokana na ucheleweshwaji wa malipo kuanzia Februari hadi Agosti mwaka 2012.
“ZRB imekuwa ikiwakumbusha Precision Air Service Co. Ltd mara kwa mara ili kulipa deni hilo, lakini wameshindwa na kupuuzia suala hilo. Sheria inatutaka kufuata utaratibu wa kukusanya na kulinda mapato ya Serikali,” alieleza.
Faki alisema Precision Air iliteuliwa na Waziri wa Fedha kukusanya malipo ya huduma na usalama kwenye uwanja za ndege wa kimataifa wa Zanzibar, chini ya kifungu namba 2 ya mwaka 1999 na sheria namba 34 ya mwaka 2007.
Alisema tabia ya makusudi ya kupuuza na kuacha kufanya mawasiliano ya kiofisi na kutolipa malipo ya ada, inayofanywa na kampuni hiyo, ni uvunjwaji wa Sheria ya Ukusanyaji wa Mapato ya mwaka 2009, gharama za huduma za ndege ya mwaka 1999 na gharama za huduma ya uwanja na wakala wa usafirishaji ya mwaka 2007.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara cha Precision Air, Patrick Ndekana, alipoulizwa alisema sio kweli kuwa ndege zao zimefungiwa.
“Sio kweli kuwa ndege zetu zimezuiliwa kutua na kuruka Zanzibar. Mpaka muda huu ninaozungumza nawe (saa 11 jioni) kuna ndege yetu inajiandaa kuruka kutoka Zanzibar,” alisema Ndekana.
Kuhusu kudaiwa zaidi ya bilioni 37.2, Ndekana alisema hana taarifa na kuongeza kuwa hilo ni suala la watu wa fedha na kuahidi kulitolea ufafanuzi zaidi.
source zero99



Love to hear what you think!