Sunday, January 20, 2013

SAKATA LA GESI: MTWARA NI MABOMU NA RISASI ZA MTOTO



MABOMU na risasi za moto jana zilitawala katika mji wa Mtwara na vitongoji vyake baada ya wananchi kufanya maandamano makubwa kupinga ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam.

Maandamano hayo yaliandaliwa na Chama Cha Wananchi (CUF) na kuongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, Julius Mtatiro, ambaye alifuatana na wabunge wa chama hicho wanaotoka mikoa ya kusini.

Maandamano hayo yamefanyika baada ya maandamano mengine makubwa yaliyofanyika Desemba 27 mwaka jana kwa lengo hilohilo, yakiwa yamendaliwa na vyama vinane vya siasa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka mkoani humo, maandamano ya jana yalifanyika huku wanawake wakiwa mstari wa mbele.
Chanzo cha kupigwa mabomu hayo kinaelezwa kuwa ni kukatika kwa umeme katika eneo ulikokuwa unafanyika mkutano wa hadhara wa CUF ambako wananchi waliahamaki na kuandamana kwenda ofisi za Tanesco Mtwara i kujua chanzo kukatika kwake.

Wakiwa njiani kuelekea Tanesco umati huo mkubwa wa wafuasi wa CUF ulikutana na Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao waliamua kuwatawanya kwa mabomu na kupiga risasi za moto hewani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mtatiro jana, lengo la kufanya maandamano na mkutano huo lilikuwa ni kupokea karatasi ya kupinga ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam
Alisema akiwa katika mkutano huo alipokea saini 10,000 za wananchi wa mikoa ya kusini ambao wanapinga mpango huo wa serikali kuisafirisha gesi. 

Maandamano hayo yalihitimishwa na mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara na wabunge wa CUF waliokuwapo ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora, Magdalena Sakaya (Tabora), Mbunge wa Mkanyageni Habib Mnyaa, Salum Barwan (Lindi Mjini), Said Bungara "Bwege" Kilwa Kusini na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mtwara, Clara Mwituka.

Mtatiro alisema msingi wa hoja yao ni kujikita katika kuhakikisha gesi inatumika kwa faida ya taifa lakini kwa kutoa kipaumbele katika maeneo yaliyo nyuma katika maendeleo, kama kusini.

Watu wakamatwa mitaani
Kutokana na vurugu hizo inaelezwa kuwa zaidi ya watu 20 walitiwa mbaroni na jeshi la polisi. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki hakuweza kupatikana jana kwa simu yake ya kiganjani. 

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mtwara, Tutufye Mwakagamba alikiri kukamatwa kwa watu kadhaa katika vurugu hizo ingawa alimtaka mwandishi wa habari hizi amtafute baadaye.

“Ni kweli ndugu yangu kuna watu kadhaa tumewakamata katika vurugu zilizotokea leo (jana), lakini ninakuomba nitafute baadaye kwa sababu muda huu nipo katika mkutano wa CUF ambako kuna mvua kubwa inanyesha,” alisema Kamanda Mwakagamba.

Biashara zafungwa
Kutokana na maandamano hayo yaliyoambatana na vurugu biashara mbalimbali zilifungwa katika soko kuu la Mtwara na mitaani hali iliyowafanya wananchi kuwa katika wakati mgumu.

Magari ya CUF kila kona
Habari zinasema mkutano wa jana ulikuwa na shamrashara za aina yake na zaidi ya magari 14 yalisafirisha wafuasi wa CUF kutoka wilayani Tandahimba wakati magari mengine manane yalitokea wilayani Newala.

Wakati huohuo, Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile (CCM), ameibuka na kuitaka serikali kutodharau madai ya wananchi wa mikoa ya kusini kuhusu suala la gesi.

Aliyasema hayo wiki chache baada ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara kufanya maandamano ya amani kupinga ujenzi wa bomba la kusarisha gesi kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.

Dk. Ndugulile, alisema kwa mtazamo wake suala hilo lina sura mbili tofauti ambayo yote yana hoja za msingi ikiwamo umaskini wa mikoa ya kusini na tataizo la ajira kwa vijana


Love to hear what you think!