Saturday, January 12, 2013

POLISI WATANO WATIWA MBARONI KWA UPOTEVU WA MILIONI 150 KATIKA TUKIO LA WIZI LILILOTOKEA KARIAKOO HIVI KARIBUI


Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linashikilia askari Polisi watano kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa Sh milioni 150 zilizoporwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi eneo la Kariakoo.

Sambamba na askari hao pia wamekamatwa watu wawili wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo ambao ni Deogratias Kimaro (30), mkazi wa Kalakata na Kulwa Mwakabala (30) mkazi wa Kijiwesamli Ilala.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema askari hao wanashikiliwa kutokana na uchunguzi wa kina uliofanywa na jopo la upelelezi likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Kanda hiyo, Ahmed Msangi.
Alisema baada ya tukio hilo zilipatikana taarifa kwamba fedha hizo zilipotea baada ya mtuhumiwa Augustino Kayula au Frank Mwangiba, kukamatwa akiwa na bastola aina ya Browning bila fedha zilizoporwa wakati inasemekana ndiye aliyepora fedha hizo akiwa na wenzake.

Askari hawa tunawashikilia na tayari mashitaka ya kijeshi yameanza huku uchunguzi ukiendelea na utakapokamilika, tutapeleka jalada kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua za kisheria ili kuleta uwazi na uwajibikaji ndani ya jamii yetu”.

Alisema Jeshi hilo limekuwa likionesha uwajibikaji ambapo mwaka jana pekee askari 20 walichukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu.

Aidha, alisema majina ya askari hao yanahifadhiwa kwa sasa, kwa ajili ya usalama na wakati ukifika yatawekwa wazi huku polisi wakiendelea na upelelezi na gwaride la utambulisho.

Alisema baada ya tukio hilo kulikuwa na taarifa zenye kutuhumu askari hao juu ya upotevu wa fedha hizo na ndipo uchunguzi ulipoendelea ili kubaini ukweli.

“Baada ya uchunguzi wa kina na ushahidi uliokusanywa, umefanya askari hao washikiliwe na kuhojiwa … pamoja na uchunguzi askari kwanza watajibu mashitaka ya kijeshi,” alisema.

Katika tukio hilo la uporaji Desemba mwaka jana, inadaiwa Kayula na wenzake wakiwa wamepanda pikipiki mtindo wa ‘mshikaki’, walivamia duka la Kampuni ya Artan Limited na kupora Sh milioni 150, zilizokuwa zikitolewa dukani Kariakoo kwenda benki, ambapo watu watatu walipoteza maisha.

Waliopoteza maisha ni pamoja na mtuhumiwa Kayula, Sadiki Juma (38) na Ahmed Issa (55) waliopigwa risasi na majambazi katika eneo la tukio.

Katika hatua nyingine, Kova alikanusha taarifa kwamba alisema ameunda tume ya kuchunguza tukio la kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka badala yake akasema ameunda Jopo la Upelelezi.



Love to hear what you think!