MMILIKI wa gari ambalo lilikuwa likiendeshwa na msanii maarufu nchini,
Hussein Ramadhan ‘Sharo Milionea’ na kupata nalo ajali iliyosababisha
kifo chake huko Muheza, Tanga, Mohammed Ismaili maarufu kwa jina la Mudi
Suma, ameibuka na kueleza uhusiano wake na marehemu, huku akisema
amekubali hasara.
Akizungumza kwa simu kutoka Muheza jana Suma alisema hana mpango wa
kudai fidia au kupeleka malalamiko yoyote kwa ndugu wa marehemu kwa
kuwa; “Kilichotokea ni kazi ya Mungu.” “Siwezi kudai hata kidogo hivyo
ni vitu vya kupita tu. Marehemu alikuwa ni zaidi ya ndugu yangu, gari ni
kitu kidogo sana katika uhusiano tuliokuwa nao,” alisema Suma na
kuongeza kwamba hata Marehemu Sharo Milionea naye alikuwa amemwachia
mali zake kadhaa ikiwamo gari.
“Siyo gari tu alilokuwa ameniachia. Kuna mikataba yake ya kazi, Bajaji
yake na funguo za chumbani kwake. Nasubiri kukabidhi vitu hivyo baada ya
kukaa na ndugu zake. Vitu viko kwenye mikono salama,” alisema.
Kuhusu gari lake lililopata ajali, Suma alisema lilikuwa na bima ndogo,
lakini anapanga kwenda TRA atakaporejea Dar es Salaam kufuatilia baadhi
ya mambo.
“Kabla ya kuondoka bima ile kubwa ilikuwa imekwisha kwa hiyo nikaamua
kuikatia bima ndogo. Nitakapofika kesho (leo) Dar es Salaam, nategemea
kwenda ofisi za bima kuzungumza nao,” alisema Suma.
Alipoulizwa kama kuna mtu mwingine atakayeathirika kutokana na gari hilo
kuharibika katika ajali mbali na yeye, alijibu: “Hakuna tofauti na mimi
mwenyewe na familia yangu.”
Kabla ya ajali
Suma alieleza kuwa kabla ya kuanza safiri yake, Sharo Milionea alifika
nyumbani kwake mchana na kumweleza kuwa afya yake haikuwa nzuri.
“Kabla ya kuondoka aliniambia kuwa hajielewi elewi na kifua kilikuwa
kinambana. Nikamshauri asiondoke peke yake, atafute mtu wa kuondoka naye
ambaye atamsaidia kuendesha gari njiani,” alisema Suma na kuongeza:
“Tulianza kuwapigia simu jamaa zetu wanne wa kusafiri naye lakini kila
tuliyemwambia hakuwa tayari. Ilikuwa ni changamoto mpaka ilipofika saa
10:45 hivi jioni, akaamua kuondoka peke yake. Wakati anatoa gari getini
kwangu, nikamwambia, basi jaribu kuwa mwangalifu sana, maana alikuwa
kweli anasumbuliwa na kifua. Tukakubaliana kwamba atakaporudi aende
hospitali kucheki afya yake.”
Kuhusu uhusiano wake na marehemu, Suma alisema: “Mimi ni mfanyabiashara
na yeye alikuwa msanii, lakini ilitokea tukawa marafiki sana mpaka
ikafikia wakati nikaona kuwa ni ndugu yangu. Nilimwamini nikamtambua
kama sehemu ya familia.”
Alisema marehemu alikuwa akitumia gari hilo kila alipolihitaji na safari
ya kwenda nalo Tanga kwa wazazi wake ilikuwa ni ya tatu.“Siyo mara ya
kwanza kuitumia gari lile, nilikuwa nimemwamini sana. Safari ya kwanza
alichukua na kusafiri nalo mwenyewe, halafu safari ya pili ikafuata na
hii ilikuwa safari ya tatu,” alisema Suma.
Eneo la ajali wakimbia makazi
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Songa Kibaoni mahala ambako Sharo
Milionea alipatia ajali, wamezikimbia nyumba zao baada ya Mkuu wa Wilaya
ya Muheza, Subira Mgalu kutoa siku moja kwa waliopora mali za marehemu
huyo kuzisalimisha mara moja