Siku moja baada ya Serikali
kutangaza kulifungia kwa muda usiojulikana gazeti la kila wiki la
MWANAHALISI linalochapishwa na kampuni ya Hali Halisi Publishers
kutokana na kulituhumu kuandika habari za uchochezi na zinazoleta hofu,
Uongozi wa gazeti hilo umezungumza.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni
hiyo Said Kubenea amesema kimsingi hawakupokea barua rasmi kutoka
Serikalini inayowataka kusitisha zoezi la kuchapisha gazeti hilo na
badala yake hizo taarifa wamezipata kupitia vyombo mbalimbali vya
habari.
Kubenea amesema hawakubaliani
na madai ya serikali kwamba gazeti hilo limekua likiandika habari za
uchochezi na kusisistiza kwamba habari yeyote inayoandikwa katika gazeti
hilo ni lazima iwe imefanyiwa uchunguzi wa kina na kamwe gazeti hilo
halikuwahi kukurupuka na kuandika habari isiyo ya kweli.
Inaaminika kwamba moja kati ya
habari za hatari zilizofanya gazeti hilo kufungiwa kwa muda usiojulikana
ni ile ya kuchapisha namba za simu za watu waliowasiliana na Dr
Ulimboka mara ya mwisho kabla ya kufanyiwa ukatili.
Kwa kusisitiza, Kubenea amesema
“hakuna kosa lolote tulilolifanya na tunastahili kupongezwa badala ya
kulaumiwa, tulichofanya sisi ni kitu kidogo sana, tuliangalia tu ni nani
aliwasiliana na Dr Ulimboka kwa mara ya mwisho… sasa tumepetaje? hizo
ni taarifa zetu, kama kuna uchochezi ambao tumeufanya tulipaswa kuwepo
Mahakamani lakini mpaka leo hatujaulizwa, hatujahojiwa, hatujaitwa hivyo
ina maana hakuna kesi…. mimi kubenea nimefanya uchochezi ni kosa,
naweza kufanya kosa kama hilo alafu natembea barabarani? “