WAKATI mgomo wa walimu ukiendelea kufukuta nchi nzima na Serikali
ikijaribu kuuzima, Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Korogwe,
anadaiwa kukamatwa kwa tuhuma za kunywa bia muda wa saa za kazi jambo
ambalo ni kinyume cha sheria.
Chanzo chetu cha habari kimesema
kwamba ofisa elimu huyo alikamatwa saa 5 asubuhi kwenye baa moja maarufu
iliyopembezoni mwa barabara kuu akiwa anakunywa pombe ambapo askari
walimkamata na kumfikisha kituo kikuu cha polisi wilayani hapa.
Kukamatwa
kwa ofisa huyo kumekuja siku moja tangu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe,
Mrisho Gambo kuamua kuingia darasani katika shule tatu tofauti na kuamua
kufundisha wakati mgomo wa walimu ukiendelea.
Mkuu huyo wa
Wilaya ya Korogwe Julai 31, mwaka huu alilazimika kuingia darasani
kwenye Shule za Msingi ya Mbeza ,Bagamoyo na Manundu akifundisha somo la
hisabati , ikiwa ni njia mojawapo ya kuwawezesha wanafunzi kusoma baada
ya walimu wao kugoma.
Jana, Gambo akizungumzia tukio la
kukamatwa kwa ofisa elimu huyo, alisema lilitokana na agizo lake baada
ya kupokea taarifa kupitia meseji ya simu ya mkononi kutoka kwa wananchi
kwamba ofisa huyo anakunywa pombe baa.
Sehemu ya ujumbe huo wa
simu ambao mwananchi imefanikiwa kuupata inasema”Inasikitisha ofisa
elimu sekondari Wilaya ya Korogwe yuko Blue Palm nyuma ya stendi
anakunywa pombe saa hizi huku walimu wakiwa wamegoma? hii ni Serikali
gani? njoo umuone”ulisema ujumbe huo wa simu ya mkononi aliyotumiwa DC.
Akithibitisha
tukio hilo mkuu huyo wa wilaya alisema:“Taarifa za ofisa elimu huyo
ninazo, mimi ndiye niliyeagiza akamatwe baada ya kupata taarifa kuwa
ameonekana anakunywa pombe muda wa kazi”alisema mkuu wa wilaya.
Mkuu
huyo wa wilaya alibainisha kwamba baada ya kukamatwa mwalimu huyo
aliagiza afikishwe hospitalini ili kupimwa lengo likiwa kuweza kubaini
kiasi cha alkoho kilichomo kwenye mwili wake ili hatua za kinidhamu za
kiutumishi zichukuliwe dhidi yake.
Aidha mkuu huyo wa wilaya
alisema kwamba baada ya vipimo hivyo kufanyika na ofisa huyo kuibainika
kwamba alikuwa na kilevi kwenye mwili wake hatua za kiutumishi
zitachukua nafasi yake ambapo pia mhusika anaweza kufutwa kazi kwa kosa
hilo.
“Nimeagiza baada ya kukamatwa ofisa huyo afikishwe hospitalini
ili kupimwa kama kwenye mwili wake kuna kilevi,na endapo itabainika
hatua kali za kinidhamu na zile za kisheria hazitasita kuchukuliwa dhidi
yake”alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine
Massawe alipotafutwa ili kuzungumzia sakata hilo simu yake ya mkononi
ilikuwa ikiita bila ya majibu ingawaje awali alisema atafuatilia na
kwenye wilaya husika na kutoa taarifa