Kocha wa Yanga Tom Saintfiet, akiwa na Kombe la Kagame wakati wakishangilia ushindi huo.
Na John JosephYANGA imetwaa ubingwa wa Kombe la Kagame 2012 juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar lakini habari ya kushangaza ni kuwa klabu hiyo imekabidhiwa kombe lenye majina ya mabingwa wa miaka iliyopita.
Katika kombe hilo, upande mmoja ulikuwa umeandikwa mabingwa wa mwaka 2006 ambao ni Polisi ya Uganda, upande mwingine limeandikwa jina la Atraco FC ya Rwanda ambao ni mabingwa wa mwaka 2009, pia upande mwingine ukiwa na heshima ya mfadhili wa michuano hiyo, Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Aidha, upande wa mwisho katika pembe nne za kombe hilo, limeandikwa jina la Yanga kuwa ni mabingwa wa mwaka 2011, kitu ambacho kinaonyesha hakukuwa na kombe jipya au pengine walilokabidhiwa halikuwa halisi.
Wakati huohuo, maandishi ya kwenye kombe hilo ya Atraco FC, Polisi na Rais Paul Kagame yote yameandikwa kwa kifaa maalum wakati upande ambao limeandikwa jina la Yanga kuwa ni mabingwa wa mwaka 2011, imebandikwa karatasi ambayo imebanduka upande mmoja na upande mwingine umechanika.
Hali hiyo inaonyesha waandaaji wa michuano hiyo, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambao rais wao ni Leodegar Tenga hawakuwa makini kufanya kazi yao, pia ubabaishaji ulichukua nafasi yake kwa kiasi kikubwa.