Joseph Mayanja Chameleone.
Jean Pierre Nimbona ‘Kidum’.
MWANAMUZIKI Mganda mwenye hulka ya utapeli, Joseph Mayanja
Chameleone, amezidi kutupambanua Watanzania. Sakata lake la kuiibia
Kampuni ya Global Publishers & General Enterprises Ltd,
limedhihirisha kuwa wana wa taifa lililokombolewa na Mwalimu Julius
Nyerere ‘JK’, hatupo wamoja.Limetoa tafsiri kwamba Watanzania wengi ni makini lakini tatizo kuna wachache ambao huamua kupotosha wengi kwa kueneza uzushi. Hao ni wale wapekepeke au viherehere, wanaojifanya wana utandawazi kwa kueneza uzushi mitandaoni.
Kundi hilo dogo la wapekepeke au mashakunaku katika muonekano wa kileo (wakijifanya wajuzi wa kutumia mitandao ya intaneti), waliwapotosha Watanzania wengi kuhusu mwanamuziki huyo tapeli, mkorofi, mwenye tamaa, mdokozi, mtukutu na maneno mengine chanya na hayo.
Wakazusha kwamba eti, Chameleone amenyang’anywa hati ya kusafiria na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric Shigongo. Yaani mtu mwenye hulka ya utapeli amezusha uongo kama ilivyo asili yake, halafu watu wachache wanashupalia kuueneza ili kupotosha ukweli.
Naomba niweke kweupe kwamba Chameleone ni tapeli. Ametenda uovu mkubwa kwa Watanzania, vilevile amemfedhehesha hata mwanamuziki mwenzake, Jean Pierre Nimbona ‘Kidum’, kwani yeye ndiye aliyesimamia malipo yote kuhakikisha kwamba Chameleone anakuja nchini kufanya shoo Julai 7, mwaka huu.
Labda nitambulishe kwamba shoo inayozungumzwa hapa ni lile Tamasha la Usiku wa Matumaini, lililofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Chameleone alikuja lakini Watanzania wengi hawatambui siri nyuma ya mwanamuziki huyo kuja nchini. Hawajui kama alishatapeli, alishaitesa na kuipa usumbufu mkubwa Global Publishers.
Wasifu wa Global Publishers katika kuihudumia jamii ya Watanzania kwa takriban miaka 15 sasa, ingetosha kuwafanya Watanzania wajiulize, kweli ni Shigongo huyuhuyu leo amegeuka mbabe, kiasi cha kumnyanyasa mwanamuziki ambaye amefanya naye kazi.
Ni suala la kujiuliza, Shigongo huyu ambaye amekuwa akiendesha harakati mbalimbali za kuwakomboa vijana, wajane, yatima na watu wa kada nyingine mbalimbali, anawezaje leo kugeuka ghafla na kuwa mkandamizaji kwa watu wengine? Swali hilo tu lilitosha kutilia shaka maneno ya Chameleone.
Ajabu ni kuwa Watanzania wanamjua mtu wao ambaye wameishi naye lakini kikundi cha wapekepeke wachache, wenye hulka ya kukenua pale wanapowaona wenzao wakiharibikiwa, ndiyo haohao wakataka kuwaambukiza ujinga Watanzania ili waamini uzushi wa Chameleone.
Mimi siamini lakini wakati mwingine huwa inaingia akilini kuwa ule msemo wa “aliye juu mngoje chini” ndiyo unaotuharibu. Kwamba mtu anayefanikiwa, usihangaike kusaka na wewe mafanikio yako, badala yake, mngoje tu chini ili muogelee pamoja kweye lindi la umaskini.
Msemo huo ndiyo umewapumbaza wengi kutoweka jitihada za kufanikiwa, badala yake wale wanaofanikiwa, watafitiniwa kwa majungu, wataombewa mabaya, watapigwa misumari ili mwisho nao waanguke. Mwisho msemo aliye juu mngoje chini utimie.
Hatutakiwi kuwa hivyo, Watanzania wanapaswa kuwa wamoja katika masuala mbalimbali. Hivi sasa, pamoja na ukweli kwamba Waganda wanamjua Chameleone alivyo tapeli, msumbufu kwa mapromota lakini bado wanamuunga mkono kwenye sakata hili.
Shigongo ambaye hajawahi kuwa na rekodi ya kuwanyanyasa wageni, kuwadhulumu malipo yao au kuwafanyia jambo lolote linalofanana na hilo, leo Watanzania wenzake wanamgeuka. Wachache wasio na uungwana wanaamua kutukana kabisa. Inashangaza kupita kiasi.
CHAMELEONE ALIFANYA UTAPELI UPI HASA? KIDUMU ALIHUSIKAJE?
Alichofanya Chameleone kinajulikana lakini kabla ya kueleza kinagaubaga, naomba nimnukuu DJ mkongwe nchini, John Dilinga Matlou ‘DJ JD’, ambaye naye aliweka wazi utapeli aliowahi kufanyiwa miaka saba iliyopita na Chameleone.
Ijumaa iliyopita, JD, aliwaeleza waandishi wa habari, waliokusanyika kwenye Hoteli ya The Atriums kwamba Chameleone siyo mtu mzuri anapokubaliana na mapromota, kwani hata yeye aliwahi kumtapeli dola za kimarekani 3,000, mwaka 2005.
Alisema: “Niliwasiliana na Chameleone moja kwa moja, akanikubalia kwenye tamasha langu lililokuwa linaitwa Wakilisha. Nilimlipa dola 3,000, baada ya kupokea fedha, hakuonekana tena na hata simu yangu akawa hapokei.
“Aliendelea kunikimbia hivyo. Tatizo kubwa lipo kwa mapromota wa Kitanzania, hatuna ushirikiano kabisa. Kila alipokuja nchini kufanya shoo, nilimfuata promota husika lakini promota mwenyewe alimficha Chameleone asikamatwe.
“Mwaka 2006, Chameleone alikuja nchini kwenye shoo fulani. Kama kawaida yake alijitahidi sana kujificha nisimfikie. Hata hivyo, pamoja na kujificha kwake, nilipewa taarifa usiku kwamba yupo Bilicanas. Nikawataarifu polisi tukaenda kumkamata.
“Chameleone aliponiona alinikimbia. Ndugu zangu, Chameleone alikimbia kama mwizi. Pale Bilicanas walikuwepo Rita Paulsen wa BSS na Merey Balhabou. Wakati polisi wamemkamata, Chameleone alikubali namdai dola 3,000 na akakubali kulipa.
“Kusikia hivyo, Rita na Merey wakaniomba nimsamehe kwa sababu mtu mwenyewe amekubali kulipa. Nikawaambia ameshanisumbua sana, Merey akasema kama hatalipa, basi yeye atamlipia. Akanisihi sana kuwa mimi ni mtu wa Morogoro mwenzake, kwa hiyo nimuache Chameleone.
“Nilikubali walichokisema lakini kuanzia hapo, Chameleone na Merey hawakupatikana. Merey alikuwa ‘bize’ na mambo yake, wakati Chameleone hakutaka kupokea simu yangu kabisa.
“Siku moja nilibadilisha namba ya simu nikampigia Chameleone, akapokea vizuri. Nikamkumbusha kuhusu fedha zangu, akaniambia hana uwezo wa kulipa ila anachoweza kufanya ni mimi kuandaa shoo nyingine halafu yeye atakuja ku-perform.
“Pamoja na kuahidi, kila nilipoandaa shoo, ukifika muda wake wa kuja hakufanya hivyo. Hii inamaanisha kuwa Chameleone ana tabia ya utapeli na Watanzania tunapaswa kuwa wamoja kwenye hili tatizo.”
JD alibainisha kuwa ameamua kutokeza na kueleza haya kipindi hiki ili kila mtu atambue kwamba Chameleone siyo mtu mzuri kwenye fedha na anaweza kumkana promota wakati wowote.
ITAENDELEA