Haruni Sanchanwa na Makongoro Oging’
MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu Cha Usimamizi wa Fedha, (IFM) jijini Dar es
Salaam, Agnes B. King’unza (pichani), amefariki dunia katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili baada ya kuokotwa akiwa hajitambui katika ufukwe
wa Bahari ya Hindi jirani na Coco Beach.
Habari za kipolisi zinasema
Agnes alitekwa kisha akaokotwa na msamaria mmoja ambaye kwa taarifa za
awali anatajwa kuwa ni mlinzi wa nyumba moja maeneo ya Coco Beach,
ambako ndiko alikokutwa akiwa hajitambui.
“Polisi na hata watu
wengine wanahisi kuwa msichana huyo alitekwa kisha kutupwa na watu
wasiofahamika, baada ya kufanyiwa ukatili wa kutisha kwa kunyweshwa kitu
kinachodhaniwa kuwa ni sumu,” kilisema chanzo chetu cha habari ndani ya
jeshi la polisi.
Habari zinasema baadaye mwanafunzi huyo ambaye
alikuwa akichukua shahada ya mambo ya kodi, alipelekwa Kituo cha Polisi
cha Oysterbay kisha askari hao wakamkimbiza Hospitali ya Agha Khan kwa
matibabu.
Hata hivyo, habari zinasema madaktari wa Agha Khan baada
ya kuona hali ya mgonjwa ilikuwa mbaya, walimpa rufaa na kumpeleka
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
“Agnes alifariki jioni ya Julai 16, mwaka huu katika Hospitali ya
Muhimbili na habari za kifo chake zilisababisha Chuo cha IFM kuzizima
kwa wanafunzi kumlilia mwenzao,” kilisema chanzo hicho.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na akasema kwamba wasamaria wema
walisema waliona Bajaj ikifika eneo alilotupwa Agnes wakadhani wanatupa
mzigo.
“Walipokwenda kuangalia wakakuta ni mtu akiwa hoi hajitambui.
Baada ya kupelekwa hospitali siku ya pili alikuja mama mdogo wa
marehemu Agnes aitwaye Veronica Galus na akaleta taarifa kuwa binti yao
huyo amefariki dunia. Polisi tunaendelea na uchunguzi kuwatafuta
wahusika,” alisema Kenyela. Hata hivyo, kifo hicho kimeacha maswali
mengi kuwa binti huyo alilishwa nini na nani?
Mzazi wa marehemu
aliyetajwa kwa jina la Bernad King’unza mkazi wa Kimara Dar,
hakupatikana kwa maelezo kwamba alikuwa safarini Iringa kwenye mazishi
ya mpendwa wao huyo yaliyofanyika nyumbani kwao Kalenga, Iringa Julai
19, mwaka huu.