CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimedai kugundua mbinu zilizotumiwa na mtoto wa kigogo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) za kuingilia mawasiliano ya simu za wabunge wake kutuma ujumbe wa vitisho kwa mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mjumbe wa Kamati Kuu wa CHADEMA, Mabere Marando, alisema mtoto huyo wa kigogo ambaye hakumtaja jina, alinunua mitambo hiyo kutoka nchini Israel.
Alisema nchini Israeli kuna kampuni mbili alizozitaja kwa majina ya Nice System na Verinty System, ambazo zimefanikiwa kutengeneza mitambo yenye uwezo wa kuingilia mawasiliano ya mtu kwa umbali wa kilometa tano na kwamba moja ya mitambo hiyo ndiyo iliyotumiwa kusambaza ujumbe mfupi wa simu kwa Mwigulu, zikionyesha kuwa zimetoka kwa wabunge wa CHADEMA.
Aliongeza kuwa mfumo uliotumika kuingilia mawasiliano ya wabunge wa CHADEMA unaitwa sms proofing, na kwamba inaweza kutumiwa na idara za kiusalama kwa sababu maalum tu.
“Tuliwauliza wabunge wetu kama wamefanya suala hilo na wakatuhakikishia kuwa hawahusiki, tukashtuka na kama mshauri wa masuala ya kiusalama wa chama tukaamua kuingia kazini kufuatilia hili, tulichogundua ni kwamba mipango hii iko nyuma ya mtoto wa kigogo wa CCM ni mtaalamu wa mitandao na ana fedha nyingi za kufanyia kazi hii,” alisema Marando.
Alieleza kuwa jambo la kusikitisha ni taarifa walizozipata kuwa mwanasheria mkuu wa serikali Jaji George Werema kuwaagiza watumishi wa ofisi yake kuandaa mashtaka kwa ajili ya tukio hilo la kuwahusisha wabunge wa CHADEMA na meseji hizo badala ya kushughulika na watu walioingilia mawasiliano yao.
Alisema kwa nafasi yake, Werema kama msimamizi mkuu wa sheria nchini anajua wazi kuwa kuingilia mawasiliano ya mtu mwingine ni kosa la jinai na mhusika anayefanya hivyo anapaswa kushtakiwa.
“Kitendo cha Jaji Werema kutoa maagizo ya kuandaa mashtaka kwa wabunge ni kuwasaidia wahalifu; tunachoweza kumuambia ni kwamba taarifa tunazo tutakutana mahakamani kuweka masuala haya wazi,” alisisitiza.
Alisema CHADEMA haitajishughulisha kulifikisha suala hilo mahakamani bali wanasubiri waitwe ili wakaudhihirishie umma namna viongozi wa CCM na watendaji wengine serikalini wanavyotumia vibaya nafasi zao kuwanyamazisha wapinzani wao kisiasa.
Alibainisha kuwa serikali ya CCM isidhani kuwafunga mdomo wakosoaji wake wa sasa ni suluhisho la ushindi kwao kwamba harakati za kudai uhuru wa kweli hazikuanza sasa na hazitaishia kwa kuwadhuru watu.
Wiki iliyopita mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu, alisimama bungeni na kuomba mwongozo wa Spika akidai kuwa amepokea ujumbe mfupi wa simu kutoka kwa baadhi ya wabunge wa CHADEMA, akitishiwa kuuawa.
SOURCE TANZANIA DAIMA!