Tausi Ally
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam,
imemhukumu kifungo cha miaka 18 jela Kada wa CCM, Rajabu Maranda na
binamu yake, Farijala Hussein katika kesi ya tuhuma za kuchota Sh2.2
bilioni za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
Mahakimu wawili katika jopo la waliokuwa wakisikiliza
kesi hiyo waliwatia hatiani watuhumiwa kwa makosa sita kati ya saba
yaliyokuwa yakiwakabili na kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu jela kwa
kila kosa.
Kwa upande wake kiongozi wa jopo hilo, Jaji Fatuma
Masengi aliwaachia huru washtakiwa hao kwa maelezo kwamba upande wa
mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka yote saba yaliyokuwa
yanawakabili.
Hata hivyo, hukumu hiyo haikuweza kuwaokoa
watuhumiwa na hasa Farijala na Maranda watatumikia adhabu yao kwa miaka
mitatu jela kwa kuwa adhabu zote walizopewa zitakwenda kwa wakati mmoja.
Tayari
Maranda na Farijala wanatumikia kifungo kingine cha miaka mitano jela,
baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh1.8 bilioni za EPA, ambapo
walihukumiwa na mahakama hiyo Mei 23, 2011.
Jopo lagawanyika
Jopo
la mahakimu watatu lililokuwa likisoma hukumu hiyo liligawanyika na
kusoma hukumu mbili tofauti, ambapo hukumu moja iliyoandaliwa na kusomwa
na kiongozi wa jopo hilo, Jaji Masengi aliyewaachia huru washtakiwa.
Hata
hivyo, katika hukumu ya pili, iliyoandaliwa na Hakimu Projestus Kahyoza
na mwenzake Catherine Revocate iliwatia hatiani washtakiwa katika
makosa sita kati ya saba yaliyokuwa yakiwakabili, na kuwahukumu kifungo
cha miaka mitatu kwa kila kosa.
Hata hivyo, wakati wakisoma
hukumu hiyo, mahakimu hao walisema badala ya washtakiwa kutumikia
kifungo cha miaka 18, hukumu yao itaenda sambamba hivyo watatumikia
kifungo cha miaka mitatu jela.
Kabla ya hukumu
Kabla ya
hukumu hiyo kutolewa, hakimu Kahyoza na mwenzake walipitia ushahidi
uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashtaka akiwamo mtaalamu wa
maandishi, Joseph Mgendi ambaye aliweza kuangalia saini katika nyaraka
halisi na zinazodaiwa kughushiwa, ikiwamo hati ya usajili ambapo
alibainisha kuwa zilikuwa zimeghushiwa.
Pia walipitia utetezi
uliotolewa wa mshtakiwa Maranda, ambaye aliyakana mashtaka yote saba
yanayowakabili na kwamba, alikataa katakata kuwa hakuwahi kula njama na
kughushi hati ya usajili wa Kampuni ya Money Planners & Consultant.
Hakimu
Kahyoza alisema, Maranda alidai kuwa yeye hakuwahi kwenda Brela
kusajili kampuni hiyo na kwamba, aliyewahi kwenda kusajili kampuni ni
binamu yake, Farijala.
Hakimu Kahyoza alisema, Maranda katika
utetezi wake alisema yeye hakuwahi kughushi hati yoyote hivyo, haikuwa
rahisi kwake kutoa hati iliyoghushiwa pia, hakuwahi kuiba fedha BoT na
wala hakuwahi kujipatia fedha yoyote kwa njia ya udanganyifu.
Kahyoza
alifafanua kwamba, Maranda alidai mfumo uliotumika kuwaingizia fedha
kwenye akaunti yao iliyopo katika Benki ya CBA uliendeshwa kihalali
ndiyo maana, BoT hawakuwahi kulalamika hivyo, aliiomba mahakama imuone
hana hatia.
Akisoma utetezi uliotelewa na Farijala, Hakimu
Kahyoza alisema, Farijala naye alikataa madai ya kughushi, kuwasilisha
nyaraka bandia benki, kuiba fedha yoyote na kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu na aliiomba mahakama imwachie huru kwa sababu hana hatia.
Yasiyo na utata
Hakimu
Kahyoza alisema kuwa mahakama ilibaini kuwapo kwa masuala yasiyokuwa na
utata ambayo ni pamoja na kwamba Maranda na Farijala ni ndugu, waliwahi
kufanya biashara pamoja na waliingiziwa fedha kwenye akaunti namba
0101379004 ya United Bank of Africa ambazo ni kiasi cha Sh2.2 bilioni.
“Baada
ya kuweka msingi huo, mahakama ilijiuliza je, washtakiwa walikula njama
ya kuiibia BoT, walighushi hati ya usajili wa kampuni namba 150731,
walighushi hati ya mkataba kati ya Kampuni ya Money Planners &
Consultant na Kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani, waliwasilisha
nyaraka za kughushi benki, waliibia BoT na kwamba je, walijipatia fedha
kwa njia ya udanganyifu,” alihoji Kahyoza.
Hakimu huyo alisema
kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa, hakuna utata kuwa hakuna mahali
panapoonyesha washtakiwa ndiyo walikuwa wamiliki wa kwanza wa kampuni
hiyo Money Planners & Consultant na kwamba majina yanayodaiwa kuwa
ni wamiliki wa kampuni hiyo ya Thobias Kitunga na Paulo ni majina ya
uongo na ya kufikirika.
Alisema licha ya majina hayo kuwa ya
kufikirika, mabadiliko ya kampuni hiyo ya Money Planners &
Consultant hayakuwahi kufanyika na hata Brela hakuna kumbukumbu, hivyo
saini zilizopo katika nyaraka za kampuni hiyo ikiwamo hati ya usajili ni
za kughushi.
Alisema sababu ya kuthibitisha hilo ni kwamba,
ofisi ni ileile iliyopo Magomeni Mapipa, Mtaa wa Iramba nyumba namba 7
hata baada ya mabadiliko.
“Hati hizo za usajili hazikusainiwa na
Msajili wa Biashara toka Brela, Noel Shani bali zilisainiwa na
washtakiwa wenyewe. Hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 333 na 335 (c) (e)
vimetufanya tufikie hitimisho kuwa washtakiwa walighushi nyaraka hizo,”
alisema Hakimu Kahyoza.
Alisema Maranda na Farijala walighushi
hati ya mkataba ya Septemba 8, 2005, wakitumia majina ya Thobiasi na
Paul na kwamba hati hiyo haikusainiwa na Kampuni ya Money Planners &
Consultant.
“Maombi ya kupewa fedha hizo Sh 2.2 bilioni,
yalipitiwa na watu kadhaa wakiwamo Mwanasheria wa BoT na kupeleka
kibali cha mwisho kwa Gavana aidhinishe malipo, hakuna hata mmoja
aliyebaini kuwa katika hati ya mkataba kati ya Kampuni ya B. Grancel ya
nchini Ujerumani na Kampuni ya Money Planners & Consultant, haikuwa
na saini ya Kampuni ya Money Planners & Consultant,” alisema.
Aliongeza:
“Kwa sababu hiyo inaonyesha wazi, washtakiwa ndiyo walighushi nyaraka
hizo hivyo hati ya usajili wa kampuni hiyo, hati ya mkataba ni za
kughushi.”
“Tuna haki ya kuamini kuwa washtakiwa kwa kujua,
walifanya hivyo kwa nia mbaya ya kuwasilisha hati hizo za kughushi CBA
na baadaye BoT”, alisema Kahyozi.
Alisema hakuna ubishi kuwa
hakuwapo hata shahidi mmoja aliyewahi kuthibitisha kuwa washtakiwa hao
waliwahi kuiibia BoT Sh 660,210,000.
“Katika hili hatupo tayari kukubaliana na upande wa mashtaka kwa sababu halijathibitika”.
Aliongeza
kwamba, hakuna utata kuwa BoT iliweka kwenye akaunti ya washtakiwa
zaidi ya Sh2.2 bilioni na kwamba, kiwango hicho cha fedha kiliwekwa
baada ya washtakiwa kuwasilisha hati za kughushi katika benki hiyo kuu
ikiwamo hati ya usajili na hati ya mkataba.
Hakimu alisema
kulikuwapo na maofisa wa juu BoT waliotakiwa walithibitishe hilo,
lakini, Mwanasheria wa BoT yeye alikuwa anathibitisha uhalali wa hati
hiyo ya mkataba ambayo haikusainiwa upande mmoja na Kampuni ya Money
Planners kuwa, “Ina nguvu kisheria hivyo, inaweza kutumiwa na BoT
kuhamisha au kuchukua fedha zinazoongelewa katika maombi ya
washtakiwa”.
Alifafanua hakimu, “Mwanasheria alimaanisha kuna
watu wengine walithibitisha, sisi kwa mtazamo wetu ni ajabu kwa maofisa
hao hata mmoja hakuwahi kuona katika hati ya mkataba hakuna saini ya
Kampuni ya Money Planners.
Tunajiuliza walimezwa katika huu
mtego au walipumbazwa? Kama walipumbazwa, upumbazo huo ulikuwa ni wa
hali ya juu na kujikuta wote wanaingia kwenye mtego huu.” alisema Hakimu
Kahyoza.
Aliongeza kwamba washtakiwa hao walifanya matendo hayo yote kwa nia mbaya na kuwafanya watu wengine, wawe sehemu ya kughushi.
Kuhusu
shtaka la kula njama, kwa ujumla maelezo yote yanaonyesha Maranda na
Farijala, walikubaliana makazi ya ofisi yawe Magomeni, Mtaa wa Iramba
nyumba namba 7 ambako ni nyumbani kwao, waliwasiliana, walikutana,
walijadiliana hivyo walitenda kosa la kula njama.
“Sisi hatuna
sababu za kusitasita kuwa kweli washtakiwa walikula njama dhidi ya BoT.
Ni kweli walikula njama,” alisisitiza Kahyoza.
Jaji Masengi
Kwa
upande wake, Jaji Masengi aliwaachia huru washtakiwa wote kwa sababu
upande wa mashtaka ulishindwa kuyathibitisha mashtaka yote saba
yanayowakabili.
Jaji Masengi alisema BoT ndiyo wangekuwa
walalamikaji wakuu, lakini haikuwahi kulalamika kutoa fedha hizo
zinazodaiwa kuibwa na washtakiwa wala Kampuni ya B. Grancel ya nchini
Ujerumani.
Kuhusu kughushi, alisema ushahidi uliotolewa
haukutosheleza kuthibitisha kosa hilo na kwamba licha ya utetezi kuwa na
upungufu lakini hakukuwa na sababu za kuwatia hatiani.
Kabla ya hukumu
Kabla
ya kusomwa kwa hukumu ya Hakimu Khayoza na Hakimu Catherine, Wakili wa
Serikali, Alapha Msafiri aliiambia mahakama kuwa washtakiwa siyo
wakosaji wa mara ya kwanza, wanatumikia kifungo cha miaka mitano jela
katika kesi namba 1161 ya mwaka 2008.
Msafiri aliiomba mahakama
itumie kifungu cha 348 na 358 cha Makosa ya Jinai (CPA), kutoa amri
Maranda na Farijala walipe fidia au warejeshe kiasi walichojipatia kwa
njia ya udanganyifu.
Wakili Majura Magafu, anayewatetea Maranda
na Farijala, alidai kuwa ni kweli washtakiwa walitiwa hatiani lakini,
isiwe kigezo cha kuwapa adhabu kali kwa sababu kesi namba 1163 na 1161
zilifunguliwa siku moja, zinahusu makosa ya aina moja isipokuwa
zilipangiwa jopo tofauti.
“Hii ni tofauti na mtu aliyetenda kosa
akaachiwa halafu akafanya tena kosa lingine, pia mazingira ya mashtaka
yanayowakabili washtakiwa yalikuwa na utata kwa namna moja au nyingine
na kwamba washtakiwa walitenda makosa bila ya kujua kama wanatenda
makosa,” aliwatetea wakili huyo na kuongeza:
“Kwa hiyo ni
dhahiri, matukio hayo hayakufanyika kwa makusudi kwa asilimia 100, kwa
kuwa wao waliamini ni halali lakini baadaye ilibainika kuwa si halai”.
“Waheshimiwa
washtakiwa wote wana matatizo ya kiafya, Farijala ana matatizo ya
presha ya macho na Maranda ana tatizo la Figo, naomba kama mahakama
itaridhia chini ya kifungu cha 38, ina mamlaka ya kuangalia mazingira ya
utendwaji wa matukio, hali za watuhumiwa na kuwaachia kwa masharti
maalumu kutokana na afya zao,”alisema Magafu.
Pia aliiomba
mahakama itamke wazi wazi kuwa adhabu watakayopewa washtakiwa kama
itakuwa ni ya kifungo, inastahili kuanza lini kwa sababu kumekuwapo na
utata wa sheria, kuwa ni lazima wamalize kifungo cha awali ndiyo waanze
kingine.
Kwa upande wa Hakimu Catherine Revocate, alisema
wamejadiliana kwa kuangalia mazingira ya kesi, afya za washtakiwa na
kwamba ni wakosaji wa mara ya kwanza kwa sababu kesi hiyo inasimama peke
yake, katika shtaka la kwanza hadi la saba kasoro shtaka la sita
waliloachiwa huru; washtakiwa hao watatumikia kifungo cha miaka mitatu
katika kila kosa.
Pia alifafanua kuwa badala ya washtakiwa hao
kutumikia kifungo cha miaka 18 katika mashtaka sita yanayowakabili,
kifungo hicho kitakwenda sambamba hivyo watatumikia kifungo cha miaka
mitatu jela.