Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelifungia
kutochapishwa gazeti la MwanaHalisi kuanzia 30 Julai, 2012 kwa muda
usiojulikana kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala za
uchochezi, uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi
kukosa imani na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani na
mshikamano uliopo nchini.
Katika matoleo yake hivi karibuni, gazeti la MwanaHalisi toleo Na.
302 la Jumatano Julai, 11 – 18, 2012 na toleo Na. 303 la Jumatano Julai
18 – 24, 2012 na toleo Na. 304 la Jumatano Julai 25 hadi 01 Agosti, 2012
na mengine yaliyotangulia yamekuwa yakichapisha habari na makala zenye
kueneza na kujenga hofu kwa jamii.
Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi, ameitwa na kuonywa mara nyingi,
lakini hataki kukiri kuwa maudhui ya makala zake hazina tija kwa jamii,
pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Mhariri, mara zote katika utetezi wake amekuwa akinukuu kifungu cha
18 cha Katiba ya nchi yetu ambacho kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kwa
makusudi kutonukuu kifungu cha 30 cha Katiba hiyo kinachoweka ukomo wa
uhuru.
Uamuzi wa Serikali
Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana
gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976,
kifungu Na. (25) (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa
mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 258
lililochapishwa katika Gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar Es
Salaam tarehe 27 Julai, 2012.
Serikali inawataka wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia
sheria, uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari
katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani
kwa wananchi.
Kama ilivyoelezwa Bungeni wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivi karibuni waandishi na
watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha kuwa habari wanazoziandika
na vipindi wanavyoandaa vinazingatia taaluma na kuweka mbele maslahi ya
Taifa letu na uzalendo. Uhuru na haki ya vyombo vya habari uendane na
wajibu.
Kuanzia sasa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya
habari ambavyo kwa maksudi vitatoa taarifa za uchochezi ambazo
zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini mwetu.
Imetolewa na
OFISI YA MSAJILI WA MAGAZETI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
30 Julai, 2012