Daniel Mjema,Moshi
POLISI katika mji mdogo wa Himo, mkoani
Kilimanjaro, wamefanikiwa kulikamata gari aina ya Toyota Noah,
linalomikiwa na askari mmoja wa polisi likiwa na shehena ya pembe za
ndovu.
Taarifa za uhakika zilizopatikana jana, zilisema gari
hilo linalomilikiwa na askari polisi mwenye cheo cha koplo lilikamatwa
saa 2:00 asubuhi nje kidogo ya mji wa Himo.
Ofisa mmoja
mwandamizi wa polisi, aliliambia gazeti hili kuwa gari hilo lililokuwa
na abiria 10, liliondoka katika mji mdogo wa Tarakea wilayani Rombo,
kwenda mjini Moshi.
Alisema baaada ya kufika eneo hilo,
lilisimamishwa na polisi wa kikosi cha kudhibiti magendo wakishirikiana
na trafiki na lilipopekuliwa lilikutwa na vipusa hivyo.
“Hizo
pembe zilikuwa kwenye mifuko ya kuhifadhidia mboea, hivi
tunavyozungumza gari limeletwa hapa kituo cha kati cha polisi na abiria
waliokuwa katika gari hilo wanahojiwa,”alisema.
Wilaya ya Rombo
inapakana na Hifadhi ya Taifa ya Tsavo, nchini Kenya na haikufahamika
kama nyara hizo za Serikali zilitokea huko au katika hifadhi ya jirani
ya Amboseli nayo ya Kenya.
Hata hivyo wakati gari hilo
likikamatwa, polisi huyo anayefanya kazi katika Kituo cha Polisi cha
Tarakea, hakuwamo katika gari hilo lakini baada ya kuarifiwa alitoa
ushirikiano kwa polisi.
Taarifa nyingine zilisema awali polisi
walikuwa wamedokezwa kuwa gari hilo lilikuwa libebe waharamiaji haramu
kutoka nchini Somalia, lakini hadi kufika subuhi mtego haukufanikiwa.
Kamanda
wa Polisi mkoani ilimanjaro, Robert Boaz, alikiri kuwapo kwa tukio hilo
lakini akaahidi kulitolea ufafanuzi kwa njia ya ujumbe mfupi (sms) kwa
vile alikuwa ziarani.
“Hilo tukio lipo lakini kwa sasa niko kwenye msafara ngoja nikuandikie kwa meseji” alisema Kamanda Boaz .